Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha ya Serikali Ludovick Utouh akifungua mkutano wa maelekezo ya ukaguzi maalum katika Manispaa ya Bukoba
Madiwani wa Manispaa ya Bukoba wakisiliza maelekezo ya CAG wakiongozwa na Meya wa Manispaa hiyo Mstahiki Antory Amani
--------------------------------------------------
Na Angela Sebastian, Bukoba
Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha za Serikali Bw. Ludovick Utouh amewasili mkoani Kagera kwa ajili ya kufanya Ukaguzi maalum katika Manispaa ya Bukoba ili kutafuta ufumbuzi wa kutatua mgogoro uliodumu takribani miaka miaka miwili na kukwamisha maendeleo ya wananchi wa Manispaa hiyo.
Bw. Utoh mara baada ya kuwasili katika mkoa wa Kagera Septemba 30, 2013 (jana) kilifanya kikao cha ufunguzi wa Ukaguzi Maalum katika Manispaa ya Bukoba na kufafanua madhumuni ya Ukaguzi huo ikiwa ni pamoja na ni namna gani ukaguzi huo utafanyika.
Bw. Utouh alisema chimbuko la Ukaguzi Maalum lilitokana na hoja zilizojitokeza baada ya kutokea kutoelewana baina ya Waheshimiwa Madiwani wa Manispaa ya Bukoba ambapo ilisababisha mgawanyiko mkubwa wa makundi na kuchangia kuzorotesha utendaji kazi wa Manispaa hiyo. Hoja hizo kuu zikiwa ni pamoja na kukosekana kwa uwazi kuhusu miradi ya uwekezaji ilivyopatikana, Mstahiki Meya kufanya maamuzi yake binafsi bila kushirikisha maamuzi ya Waheshimiwa Madiwani kupitia Baraza la Madiwani.
Akifafanua kifungu cha sheria kinachompa mamlaka ya kufanya ukaguzi maalu Utouh alisema, “Kwa mujibu wa kifungu cha 36 cha sheria ya Ukaguzi wa Umma Na. 11 ya mwaka 2008, Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali anayo mamlaka ya kufanya ukaguzi pale atakapoona kuwa inafaa katika masuala yanayohusiana na fedha na mali za Umma.”
Aidha Bw Utouh alieleza kuwa alichelewa kufika katika Manispa ya Bukoba kufanya Ukaguzi Maalum ili kufanya maandalizi ya kutosha kabla ya ukaguzi huo ikiwemo kuuandaa Adidu za Rejea wakati wa kufanya ukaguzi huo ili kutenda haki katika pande zote mbili na kuumaliza mgogoro.
Adidu za Rejea 13 za Ukaguzi Maalum Manispaa ya Bukoba Kuchunguza usahihi wa utaratibu uliotumika kumpata mwekezaji wa kituo cha kuosha magari (ACE Chemical Ltd), Kuchunguza uhalali wa nyaraka na kiasi kilichowekezwa cha sh.297,000,000 kwenye mradi wa kuosha magari Kuchunguza tatizo na sababu zilizopelekea viwanja 800 kutogawiwa kwa wananchi waliochangia gharama za upimaji.
Pia kuchunguza wa upimaji viwanja 5,000 Kuchunguza miradi wa ujenzi wa soko, ujenzi wa kitega uchumi na kituo cha Mabasi, ujenzi wa chuo cha ualimu, ujenzi wa kituo cha maarifa na ujenzi wa Bwawa kwa ajilli ya utalii.
Na pia Kuchunguza Kiwanja cha Shule ya Msingi Kiteyagwa, Barabara ya kupitia Kagondo Kaifo hadi Kagondo Karuguru na kuchunguza masuala mengine ya matumizi ya fedha yanayoashiria ubadhirifu.
“Ukaguzi huu maalum unawagusa waheshimiwa kadhaa wenye nyadhifa za juu kisiasa na Serikalini na pia katika uongozi wa Halmashauri;kwa hiari hiyo ningependa kutoa tahadhari kubwa kwa uongozi wa Manispaa ya Bukoba na kwa wale wote wanaotuhumiwa kwa njia moja au nyingine kujiepusha na vitendo vyovyote vyenye mwelekeo wa rushwa ambavyo vinaweza kuvuruga mwenendo mzima wa ukaguzi huu maalum na kusabisha matokeo yaliyokusudiwa kushindwa kufikiwa”, alisisitiza.
“Wakaguzi hawa ni wenye ujuzi wa kutosha na wa muda mrefu msije mkajaribu kuwapelekea vibahasha mtajisumbua bure kwani hawatapokea.” Aliongeza Utouh.
Vilevile Bw. Utouh aliwaagiza Katibu Tawala Mkoa na Mkurugenzi Mtendaji wa Manispaa ya Bukoba Kuhakikisha kuwa watendaji wote waliokwishahama na watahitajika kutoa maelezo katika ukaguzi huo maalum wapatikane ili kutoa ushirikiano wa dhati.
Katika hatua nyingine Mkuu wa Mkoa wa Kagera Mhe. Kanali Mstaafu Fabian Massawe alimshukuru Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Fedha ya Serikali kufika mkoani hapa ili kutoa suruhu ya mgogoro wa muda mrefu uliokwamisha jitihada za kuwaletea maendeleo wananchi wa Manispaa ya Bukoba.
Taarifa ya ukaguzi maalum katika Manispaa Bukoba itakamilika ndani ya siku 35 kuanzia Septemba 30, 2013 na mara baada ya kukamilika taarifa hiyo itakabidhiwa Ofisi ya Waziri Mkuu ili kuwawajibisha wale wote watakaobainika kufuja fedha na mali za serikali na kuuumaliza mgogoro uliodumu miaka miwili.
0 comments:
Post a Comment