Waziri wa Katiba na Sheria, Mheshimiwa Mathias Chikawe (MB) siku ya tarehe 28/9/2013 alitembelea Gereza Kuu la Isanga Mkoani Dodoma kwa nia ya kukagua miundombinu ya Gereza na kusikiliza kero za Wafungwa na Mahabusu wa Gereza hilo.
Ziara hiyo ni mwendelezo wa Mkatati wa Wizara ya Katiba na Sheria wa kutembelea Magereza Nchini kwa lengo la kubaini na kutatua kero na changamoto ambazo zinayakumba Magereza Nchini pamoja na wafungwa na mahabusu.
Ziara hizo pia zinalenga katika mkakati wa Wizara na Taasisi zake wa kupunguza mlundikano wa wafungwa na mahabusu Magerezani na pia kupunguza mlundikano wa mashauri ya jinai Nchini. Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Chikawe aliongozana watendaji wa Serikali kutoka katika Wizara ya Katiba na Sheria, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kanda ya Dodoma, Mahakama ya Tanzania, Ofisi ya Kamanda wa Polisi,Mkoa wa Dodoma.
Mkuu wa Magereza wa Mkoa wa Dododma SACP Kibwana Mponda alimweleza Mheshimiwa Chikawe kuwa Gereza hilo lilijengwa kati ya mwaka 1946 na 1949 na lina uwezo wa kuhifadhi wafungwa 784 lakini kwa sasa lina jumla ya wafungwa na mahabusu 1149. Kwamba Gereza hilo ni moja ya Magereza Makubwa Tanzania Bara na linahifadhi wafungwa wa aina zote haswa wafungwa wakorofi na wale wenye matatizo ya akili.
Katika ziara hiyo, Mheshimiwa Chikawe alipata fursa ya kukagua miundombinu ya Gereza hilo na kuongea na wafungwa na mahabusu, ambapo alielezwa kero na matatizo mbalimbali yanayowakabili.
Wakati akiongea na wafungwa na mahabusu, Mheshimiwa Chikawe alisema ameridhishwa na miundombinu iliyopo Gerezani hapo na huduma mbalimbali wanazopatiwa wafungwa na mahabusu ingawa bado kuna haja ya kuiboresha zaidi. Pia alisema ameridhishwa na ushirikiano uliopo baina ya Idara ya Magereza ya Mkoa wa Dodoma, Mahakama, Polisi na Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali uliosaidia kuwepo kwa utatuzi wa changamoto na kero mbalimbali za wafungwa na mahabusu na kwa kiasi kikubwa ushirikiano huo umeendelea kupunguza msongamano wa wafungwa na mahabusu Gerezani hapo, alitoa mfano kuwa Msongamano umepungua kutoka wafungwa na mahabusu 2200 waliokuwepo mwaka 2007 hadi wafungwa na mahabusu 1149 mwaka 2013.
Mheshimiwa Chikawe aliahidi kuwa, Wizara kwa kushirikiana na Mahakama, Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali na Polisi kwa pamoja watazifuatilia na kutatua kero ya kutopatikana kwa nakala za hukumu na mienendo ya mashauri kwa wakati, kuchelewa kwa vitabu ‘records of Appeal’, uhaba wa vikao vya Mahakama Kuu na ucheleweshaji wa upelelezi, kero ambazo zililalamikiwa sana na wafungwa na mahabusu gerezani hapo.
Pia Mheshimiwa Chikawe aliwahakikishia wafungwa na mahabusu kuwa Serikali itaendelea na mikakati yake ya kuhakikisha kuwa msongamono wa wafungwa na mahabusu magerezani unatatuliwa, usikilizwaji wa kesi unakuwa wa ufanisi na kupunguza kwa kubambikiwaji kesi.
Mheshimiwa Chikawe (Mwenye flana nyekundu) akiwa na Viongozi wa Magereza Mkoa wa Dodoma pamoja na watendaji wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kanda ya Dodoma, Mahakama na Ofisi ya Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Dodoma mara baada ya kutembelea Gereza Kuu la Isanga.
Mheshimiwa Chikawe,akiwa kwenye picha ya pamoja na Viongozi wa Magereza Mkoa wa Dodoma pamoja na watendaji wa Serikali kutoka Ofisi ya Mwanasheria Mkuu wa Serikali Kanda ya Dodoma, Mahakama na Ofisi ya Kamanda wa Polisi, Mkoa wa Dodoma mara baada ya kutembelea Gereza la Wanawake la Isanga.
0 comments:
Post a Comment