Mratibu wa maadhimisho ya unywaji wa maziwa mashuleni Iringa kutoka kampuni ya Asas Bw Tony Adam katikati akizungumza na wanahabari Iringa katika ofisi za IPC juu ya maadhimisho hayo ,kulia ni katibu wa chama cha waandishi wa habari mkoa wa Iringa Bw Francis Godwin na kushoto ni afisa habari wa kampuni ya maziwa ya Asas
Wanahabari wa vyombo mbali mbali wakimsikiliza kwa makini mratibu huyo
Na Francis Godwin, Iringa
WAKATI kesho ni maadhimisho ya siku ya unywaji maziwa duniani ,kampuni ya maziwa ya Asas Dairies Limited Iringa inakusudia kuwanywesha maziwa wanafunzi 30,000 wa shule za msingi katika Halmashauri ya Manispaa ya Iringa kama sehemu ya kuhamasisha jamii kujenga utamaduni wa kunywa maziwa kwa afya .
Akizungumza na wanahabari leo katika ofisi za IPC ,mratibu wa uhamasishaji unywaji maziwa mashuleni kutoka kampuni ya ya maziwa ya Asas Bw Tony Adam alisema kuwa kuwa wakati madhimisho ya unywaji maziwa kitaifa yanafanyika katika mkoa wa Tanga ,Kampuni hiyo ya Asas Dairies Ltd yenye makao yake makuu mkoani Iringa imelazimika kufanya maadhimisho hayo mjini Iringa kwa kushirikiana na uongozi wa Manispaa ya Iringa.
Mratibu huyo alisema kuwa shule zote za Halmashauri ya Manispaa ya Iringa zitapata kupewa maziwa katika uwanja wa Samora mbele ya mgeni rasmi mkuu wa mkoa wa Iringa Dr Christine Ishengoma .
PIa alisema kuwa wanafunzi wote wa shule za msingi wenye miaka chini ya 10 watashiriki katika mashindano ya uchoraji wa picha za rangi zitakazobeba ujumbe wa maziwa kwa mfano ng'ombe akila majani ama mtoto akinywa maziwa .
Mbali ya watoto kushindana kuchora pia watu wazima watapata kushiriki semina itakayoelezea umuhimu wa unywaji wa maziwa na madhara ya kutotumia maziwa katika mwili wa binadamu na kuwa semina hiyo itahusisha pia wadau wa maziwa na viongozi wa mkoa na Manispaa ya Iringa pamoja na wawakilishi wa taasisi zinazohusika na sekta ya maziwa za zile bodi ya maziwa , lishe na chakula nchini (TFNC).
Alisema madhumuni makubwa ya madhimisho hayo ni kuamsha hisia za wakazi wa Manispaa ya Iringa kuhusu umuhimu wa unywaji maziwa katika kujenga afya ya mwili na kiakili zaidi.
Kwani alisema kuwa kiwango cha unywaji wa maziwa nchini bado ni wa kiwango cha chini sana cha wastani wa lita 40 za maziwa kwa mtu kwa mwaka ambazo zimepanda lita 60 za maziwa kwa mtu kwa mwaka ikilinganishwa na kiwango cha kimataifa (WHO) cha lita 200 za maziwa kwa mtu kwa mwaka au kiwango cha majirani zetu Kenya cha lita 120 za maziwa kwa mtu mmoja kwa mwaka .
Alisema kuwa kiwango chetu hapa nchini ni sawa na na unywaji wa maziwa cha pipa moja la maziwa kwa mtu mmoja kwa mwaka huku dhamira ya kiwanda cha Asas Iringa ni kuona kiwango hicho kinaongezeka kufikia lita 80 hadi 100 za maziwa kwa mtu mmoja kwa mwaka ndani ya kipindi cha miaka 5 ijayo.
Mratibu huyo alisema kuwa kiwanda hicho cha Asas Dairies Ltd kimeendelea kufikisha bidhaa zake kwa wananchi wengi zaidi nchini kwa kuhakikisha wanafikiwa na huduma zao na kutaja bidhaa zinazozalishwa kuwa ni maziwa fresh,maziwa mgando ,Yogurts zenye ladha mbali mbali .
Aidha ametaja kaulu mbio ya maadhimisho ya unywaji wa maziwa mashuleni katika Manispaa ya Iringa kwa mwaka huu kuwa ni UNYWAJI WA MAZIWA KILA SIKU SHULENI NI HAKI YA KILA MWANAFUNZI.
0 comments:
Post a Comment