Mwenyekiti wa soko kuu Makete mjini akizungumza kwenye ofisi za CCM.
Mfanyabiashara Mia Sanga akizungumza ya moyoni mwake.
Mfanyabiashara Andrea Sanga akiweka wazi aliyonayo
Mwenyekiti wa CCM wilaya ya Makete Francis Chaula akizungumza na wafanyabiashara hao.
======
Na Edwin Moshi,Globu ya jamii Makete
Wafanyabiashara eneo la sokoni Makete mjini ambao wanatakiwa kubomoa mabanda yao ya biashara kupisha ujenzi wa barabara kwa kiwango cha lami, wamebisha hodi kwenye ofisi za chama cha mapinduzi wilaya hiyo kupeleka malalamiko yao kufuatia kuandikiwa barua na halmashauri ambayo wamedai inawaumiza
Wakiwa katika ofisi hizo, Mwenyekiti wa soko hilo Hosea Mpandila alitoa sababu za wao kuongozana kwa pamoja hadi kwenye ofisi hizo kuwa wanasikitishwa na kitendo cha wao kuzuiwa na halmashauri kuendelea na ujenzi wa vibanda vyao kwenye eneo ambalo walipangiwa awali na halmashauri licha ya baadhi yao kupeleka vifaa vya ujenzi kwenye eneo hilo
Amesema jana waliandikiwa barua na mkurugenzi wa halmashauri ya Makete (mtandao huu unayo barua hiyo) ambayo amedai ina masharti ambayo hawawezi kuyatekeleza kwa kuwa yanawaumiza, ikiwemo la kutakiwa kuomba upya kupatiwa viwanja vya kujenga mabanda, na mabanda wakishayajenga wanatakiwa kuainisha gharama za ujenzi kwa halmashauri ambapo watakuwa wakilipa kiwango nafuu cha ushuru na kiasi kingine cha fedha kinachukuliwa na wafanyabiashara hao na wakisharudisha gharama za ujenzi, vibanda hivyo vitakuwa mali ya halmashauri na watakuwa na mamlaka ya kumpangisha yeyote wanayemuona anafaa
"Kwa kweli inatusikitisha sana, hivi inawezekanaje sisi tujenge vibanda kwa gharama zetu wenyewe halafu tuje kurejeshewa gharama kidogokidogo na zikishakamilika mabanda yawe ya halmashauri, hii ina maana gani? kama ndivyo basi halmashauri ijenge vibanda itupangishe sisi" alisema Andrea Sanga
Mwingine aliyejitambulisha kwa jina la Mia Sanga amepinga uamuzi wa wao kuomba upya kupewa viwanja hivyo wakati wote walishapimiwa na serikali na kuruhusiwa kuendelea na ujenzi, na kuitaka serikali kuwarejeshea kama walivyowapa awali ili waendelee kujenga kwa kuwa muda waliopewa wa kubomoa mabanda yao kwa hiari unakaribia kuisha
Akizungumza na wafanyabiashara hao kwenya ofisi za CCM wilaya hiyo, mwenyekiti wa CCM wilaya ya Makete Francis Chaula, amewapa pole wafanyabiashara hao na kushangazwa na barua hiyo waliyopewa na kuwataka kuwa na subira kwani wamefikisha malalamiko yao kwenye eneo sahihi na kuahidi kulishughulikia
Chaula amesema haimuingii akilini wafanyabiashara hao kusimamishiwa ujenzi na kutakiwa kuomba upya huku akisisitiza wao kama chama watafika kwenye ofisi ya mkurugenzi kupata muafaka wa suala hilo mara moja
Mtandao huu ulipofika kwenye ofisi ya mkurugenzi mtendaji kuzungumzia suala hilo, haukumkuta na badala yake mwandishi wetu alijibiwa kuwa mkurugenzi amesafiri kwenda Matamba kwa ajili ya kuangalai maandalizi ya kuupokea mwenge wa uhuru
0 comments:
Post a Comment