ZAIDI ya washiriki 100 kutoka ndani na nje ya nchi watashiriki kwenye tamasha la Sanaa na utamaduni la Jambo Festival litakalofanyika oktoba 23 hadi 27 mwaka huu katika viwanja vya Suye vilivyopo Arusha.
Mwenyekiti wa tamasha hilo, Augustine Namfua alisema kuwa tamasha hilo ni la pili kufanyika mkoani Arusha ambapo wamekuwa wakifanya kila mwaka lengo likiwa ni kuwawezesha washiriki mbalimbali kuweza kuonyesha bidhaa zao za kitamaduni kutoka ndani na nje ya nchi.
Alisema kuwa tamasha hilo la kimataifa pia litawashirikisha washiriki kutoka nchi za Ufaransa na Angentina ambao wataonesha mambo mbalimbali na kuonyesha bidhaa zao za kitamaduni .
Alisema tamasha hilo litaenda sambamba na matukio mbalimbali ya kiasili ikiwemo maonyesho ya mavazi ya kiasili, pamoja na tamasha la kiasili kutoka vikundi vya miji ya Tanga, Arusha, na Dar es Saalamu .
Namfua aliongeza pia kutakuwepo na tamasha la muziki wa kisasa pamoja na onesho la mavazi, na ubunifu wa mavazi ambapo kwa siku hizo kila siku kutakuwa na matamasha mbalimbali.
Amesema maandalizi ya tamasha hilo yamekamilika kwa asilimia 50 huku watu mbalimbali wakiwemo watu binafsi, mashirika na taasisi mbalimbali zinazohusika na maswala ya sanaa na tamaduni wanaendelea kujitokeza kwa wingi kwa ajili ya kushiriki.
"Tamasha la mwaka jana lilifana sana kwani tuliweza kupata washiriki wengi sana kutoka ndani na nje ya nchi na lilikuwa na mwitiko mkubwa sana , huku watu mbalimbali wakipata fursa ya kuonyesha sanaa zao na tamaduni mbalimbali na kuweza kujifunza kutoka kwa wenzetu wa nje ya nchi ndio maana tumeamua kufanya tena mwaka huu mwezi wa kumi hivyo tunatarajia watu mbalimbali kushiriki kikamilifu katika tamasha hilo’alisema Namfua.
Aidha aliwataka watu mbalimbali kufika katika tamasha hilo na kuonyesha bidhaa zao za kitamaduni zinazotengenezwa kwa mikono pamoja na kutangaza tamaduni zao za Kiafrika na kuwataka wadau mbalimbali kuonyesha moyo katika kusaidia matamasha hayo ili yaendelee kufanyika mara kwa mara.
0 comments:
Post a Comment